Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, leo ameanza hotuba ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka 2025/26 kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa jitihada kubwa anazofanya katika sekta ya maji nchini.

Waziri Jumaa Aweso amesema ametumikia Wizara ya Maji kwa takribani miaka minane mfululizo, akisisitiza kuwa hilo si jambo dogo. Ameeleza kuwa kipindi hicho kimemjengea uzoefu mkubwa na amekuwa shahidi wa mabadiliko chanya katika sekta ya maji nchini. Akinukuu methali ya Kiswahili, alisema: “Moyo usio na shukrani hukausha mema yote”.
Waswahili husema, “chanda chema huvikwa pete”. Methali hiyo imejidhihirisha na Mataifa yameiona kazi njema ya Mheshimiwa Rais na wamemvika taji.
Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso, amesema mafanikio makubwa yamepatikana katika sekta ya maji chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan. Akizungumza bungeni, amesema Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002 imerekebishwa na toleo jipya la 2025 limekamilika, likiwa na mtazamo wa maendeleo hadi mwaka 2050 na Ajenda ya Afrika 2063.
Aweso amesema jumla ya miradi 2,331 ya maji imekamilika – 1,965 ya vijijini na 366 ya mijini, huku upatikanaji wa maji vijijini ukipanda hadi 83% na mijini hadi 91.6%. Kupitia RUWASA, vijiji 10,517 vimenufaika. Zaidi ya Shilingi Trilioni 4 zimewekezwa katika sekta hiyo.